Kwa mujibu wa Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Ahmad Al-Qattan, Mwenyekiti wa Jumuiya ya “Kauli Yetu na Matendo” na mwanazuoni wa Kisunni wa Lebanon, alianza hotuba yake katika hafla moja kwa kusisitizia dhana ya uchamungu na udugu miongoni mwa Waislamu, na akasema: "Ujumbe wa kwanza ni kudumisha mafungamano ya kifamilia na umoja wa Umma wa Kiislamu, kwa sababu nguvu ya kweli imo katika umoja na mshikamano wa Waislamu."
Akiashiria kwamba ushindi dhidi ya maadui unaweza kupatikana tu kupitia umoja wa kitaifa na Kiislamu, aliwataka Walebanon kuungana mbele ya kile alichokiita adui wa Kizayuni na Marekani.
Alisisitiza kuwa mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel dhidi ya Lebanon yanahitaji msimamo wa kitaifa ulio mmoja na wenye mshikamano.
Sheikh Al-Qattan alisisitiza kwamba; kuhalalisha uhusiano wa kawaida na kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na adui Israel, pamoja na kujisalimisha kwa matakwa yake, ni jambo la haramu kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu. Pia alisisitiza kukataliwa kwa mazungumzo yoyote ya moja kwa moja.
Mwanazuoni huyo wa Kisunni wa Lebanon pia aliutaka Umma wa Kiislamu kumtambua adui wake na kuungana dhidi yake, huku akionya kwamba; hatari ya Israel haiishii Palestina na Lebanon pekee, bali inatishia nchi zote za Kiarabu na Kiislamu, ikiwemo nchi za Ghuba ya Uajemi.
Kuhusu masuala ya Lebanon, Sheikh Al-Qattan alisisitiza kwamba; usalama na uthabiti wa Lebanon haviwezi kupatikana isipokuwa kwa mshikamano wa wananchi, jeshi na Muqawama, na akalielezea hilo kuwa ni mfumo unaoilinda nchi dhidi ya uchokozi wa nje.
Alimpongeza kila mpiganaji, shahidi na majeruhi aliopoteza maisha yake katika njia ya kuitetea Lebanon, na akaisifu nafasi ya wapiganaji na walinzi wa kusini, akiwaita “fakhari na heshima ya Walebanon.”
Sheikh Al-Qattan alituma ujumbe kwa wakimbizi wa kusini na baadhi ya vijiji vya eneo la Biqaa, akiwataka kuwa na subira na ustahimilivu, na kusisitiza kwamba; kujitolea kwao hakutakuwa bure na kwamba ushindi, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, uko njiani kuja.
Pia alielezea imani yake katika ushindi wa mataifa yanayokabiliwa na ukaliaji wa ardhi, na akaashiria kwamba; Mwenyezi Mungu hawapi ushindi madhalimu wakubwa, na kwamba ushindi utakuwa wa watu wa Palestina, Ghaza, Lebanon na kila mpinzani wa ukandamizaji katika ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu.
Sheikh Al-Qattan aliisifu Iran kwa kusimama imara mbele ya mashinikizo na uchokozi, na akasema kwamba; ushindi wake ni ushindi wa watu wote huru duniani, bila kujali dini, madhehebu au makundi yao.
Alihitimisha hotuba yake kwa maneno haya: "Ushindi uko karibu kwa idhini ya Mwenyezi Mungu." Na aliwataka Waislamu kuwa na subira, ustahimilivu na kumtegemea Mwenyezi Mungu, huku akirejea Aya Tukufu isemayo:
(إن تنصروا الله ینصرکم ویثبت أقدامکم)
"Mkimnusuru Mwenyezi Mungu naye atakunusuruni na ataithibitisha miguu yenu."
Maoni yako